Bw. Spika wa Muda, Rais alianza kwa kupongeza viongozi waliochaguliwa. Kwa hivyo, ningepeda kuchukua fursa hii kuwashukuru wananchi wa Taita Taveta kwa kunichagua tena kwa awamu ya pili kwa sababu wanaamini uongozi wangu. Pia, nachukua fursa hii kuwapa kongole Maseneta wote waliochaguliwa na wananchi na vile vile wale walioteuliwa kuwakilisha vikundi tofauti. Vile vile, nampongeza Rais kwa kuchaguliwa kama Rais wa Jamhuri ya Kenya. Watu husema kuwa katika kila mashindano, lazima kuwe na mshindi na mshinde. Katika aya ya tatu, Rais alisema kwamba Serikali yake itashirikisha maeneo yote ya Kenya katika uongozi. Alipendekeza kuwe na Mawaziri 22. Hata hivyo, kuna baadhi ya maeneo ambayo hakuna Waziri hata mmoja aliyeteuliwa. Mfano ni Kaunti ya Taita Taveta. Kusema ukweli, hatuwezi kuwa na Mawaziri kutoka kila sehemu ya Kenya. Kuna Makatibu Wakuu na pia Chief Administrative Secretaries (CASs) ambao hawajachaguliwa. Tunasubiri mahakama kuamua iwapo ni sawa kuwa na CASs. Ikiwa hivyo, namwomba Rais aangazie maeneo ambayo yaliachwa nyuma katika uongozi kama vile Jimbo la Taita Taveta ndio angalau tuwe na Katibu Mkuu au hata CAS. Bw. Spika wa Muda, aya ya 21 inaangazia mambo ya kutoa ruzuku na pembejeo, haswa mbolea. Rais aliamuru bei ya mbolea kushuka kutoka Kshs6,500 hadi Kshs3,500. Namshukuru Rais kwa jambo hilo. Jinsi wengine walivyosema, hii si mara ya kwanza kwa Rais kushukisha bei ya mbolea. Mwaka wa 2008, akiwa Waziri wa Kilimo katika Serikali ya “Nusu Mkate”, alishukisha bei ya mbolea kutoka Kshs6,000 hadi Kshs2,400. Vile vile amefanya hivyo. Kushukisha bei ya mbolea pekee hakutasaidia kuhakikisha kuna food security. Kuna maeneo kama vile Kaunti ya Taita Taveta ambayo kando na kupata pembejeo, mambo kadha wa kadha yanafaa kufanyika ili kuhakikisha kwamba kuna chakula. Kuna maeneo kama vile Wundanyi na Werugamghange ambapo tukipata mvua vizuri, tulime na tupate mbolea, basi kutakuwa na mazao. Wananchi wa huko hawavuni kwa sababu ya shida za wanyamapori kama vile tumbili. Wananchi wa Wundanyi hawawezi kulima kwa sababu ya tumbili. Kando na pembejeo, Serikali pia inafaa kujua jinsi wakulima hao watalima. Wenyewe wana bidii ya kulima lakini chakula chao chote kinaliwa na nyani na tumbili. Njia gani zinaweza kutumika kulinda chakula cha wananchi hao dhidhi ya wanyamapori kama vile tumbili na nyani? Lazima kuwe na mikakati mwafaka ya kuhakikisha kwamba nyani na tumbili wameuawa au wafungiwe mahali ili wasifike kwenye mashamba yao. Hata ukiwapa mbolea watu wa maeneo ya chini kama vile Mwatate, Voi, Taveta na mengineyo ya Wundanyi kama vile Kishushe, hawawezi kulima kwa sababu hakuna maji. Wanategemea unyunyiziaji mashamba maji. Bw. Spika wa Muda, kando na kutoa mbolea ambayo imetolewa ruzuku, lazima kuwe na mpango mwafaka wa kuleta maji katika maeneo kame ya Kaunti ya Taita Taveta. Bw. Spika, kama unavyojua, Taita Taveta, kuna vyanzo vingi sana vya maji vinavyohitaji hela kidogo tu. Kwa mfano, kuna Ziwa la Challa, Ziwa la Jipe, Mzima Springs na Njoro Springs. Hivyo ni vyanzo vya maji ambavyo Serikali ikiwekeza pesa kidogo tu kama Kshs5 bilioni hadi Kshs10 bilioni, maeneo yote ya Mwatate na Voi yatapata Maji. Tukipata pamoja na ile mbolea ambayo imetolewa ruzuku, basi wananchi wataweza kulima na kupata chakula chao cha kutosha na hata chakula cha kuuzia Kenya nzima. Maeneo ya Taita Taveta ni maeneo yanayojulikana kuwa hayana ugonjwa katika mambo ya kufuga wanyama. Yale maeneo yakipewa maji na wananchi wapande nyasi, ni maeneo ambayo tunaweza kufuga ngómbe wengi na kupata wa kutosha Wakenya na pia kuuza nchi za ngámbo na pia kuleta ajira nyingi sana. Namshukuru Mheshimiwa Raisi kwa sababu katika aya ya ishirini na nane, ameongea mambo ya kutafuta pesa kwa kima cha Kshs900 bilioni kupitia mfumo wa Public Private Partnership (PPP), ama kutumia serikali na idara ambayo si ya serikali, ili kupata pesa ya kutosha ya kupata na kupeleka maji katika sehemu kame. Hilo naliunga mkono kwa sababu maeneo ambayo yana rotuba lakini hayana maji yanaeza kugeuzwa ili tunyunyizie mashamba maji na tuache ukulima wa kutegemea mvua. Ingawaje tumejaribu hili wakati mwengine maeneo ya Kilifi, kwenye mradi wa Galana Kulalu na haikufaulu. Lakini hata kama haikufaulu huko, hatuwezi kusema kwamba haiwezi faulu hata sasa. Kama Waisiraeli walifanya na wakafaulu, basi tuwalete huku watusaidie ili tuweze kufaulu. Katika mpango wa PPP, hii miaka mitano iliyopita tulikuwa tunasukuma mapendekezo tuliyokuwa nayo. Tuliyapeleka kwa PPP department kule Treasury ila hawakupitisha huo mradi wa Njoro Kubwa uliohitaji pesa kiwango cha Kshs6 billion na ulikuwa unalipiwa na sekta ambazo si za Serikali. Najua saa hizi saa hizi utaenda kupita, kwa sababu Raisi amesema watatumia hiyo mbinu ili kupata wafadhili wa kuleta maji kupitia mpango wa PPP, ili tupate maji ya kunyunyizia mashamba yetu. Katika maeneo haya kame, wananchi wanalima lakini hawawezi kuvuna kwa sababu ya kero la ndovu na wanyama pori. Ni vizuri serikali za kaunti, Serikali ya Kitaifa na Kenya Wildlife Service (KWS) washirikiane ili waweke nyaya za stima za kuzuia ndovu wasiingie katika maeneo ambayo wananchi wetu wanalima. Lingine ni kuhusu hii Kshs50 bilioni ambayo inaitwa Hustler Fund. Hii ndio itakayobadilisha uchumi wa Kenya. Kama kila Kaunti inaweza kupata Kshs1 billion ielekezwe kwenda kwa vijana, akina mama na walemavu, wapewe tender - Seneta wa Uasin Gishu ameongea vizuri sana kuhusu hii - wapewe pesa ya kufanya miradi na kaunti. Serikali ya Kitaifa au Treasury iangazie kwamba ile pesa imelipwa katika zile tender, basi wananchi wa chini ambao ni vijana na kina mama wanaoitwa hustler, wataweza kusaidika. Lakini tukifanya kama zile pesa zingine zilivyo, kwamba zinakopwa na kufanya biashara na Kaunti na Kaunti haziliwapi, wanakuwa na pending bills, basi huu mfumo wa pesa ya hustler bado hautasaidia wananchi wetu kujikuza kiuchumi. Jukumu letu kama Bunge ni kusaidia Serikali iliyoko kutengeneza sera, sheria na kanuni mwafaka za kusaidia hii hustler fund ifanye kazi vizuri kwa manufaa ya wananchi wetu. Hivi ndivyo tutapima Serikali yetu ya Kenya Kwanza kwa sababu haya ni mawazo yao wenyewe. Jambo lingine la muhimu ni kuhusu kufufua uchumi. Tumeona kwamba uchumi umelemaa hususan katika maswala ya utalii Kaunti za pwani. Watalii wengi waliokuwa wakuja pwani wameweza kuenda katika maeneo mengine kama Zanzibar ambao ni jirani. Hii imesababishwa na kufungwa kwa viwanja vya ndege na mashirika ya ndege nchini. Kwa mfano, ukienda nchini Zanzibar kuna ndege zaidi ya kumi ambazo zinatoka nchi za kigeni kila siku. Zinaleta watalii katika nchi ile ilhali Mombasa Kaunti haina ndege hata moja na hiki ni kiwanja cha kiwango cha kimataifa. Miaka mitatu nyuma, kiwanja kile kilikarabatiwa na takriban shillingi billioni saba. Hata hivyo, hatujaona ndege zozote za kimatiafa zikishuka na kuleta watalii na kurahisisha usafiri baina ya Mombasa na miji miingine mikubwa ulimwenguni. Usafiri wa ndege; kwa watalii wa humu nchini, umekuwa ghali kwa sababu Kenya Airways ambalo ndilo shirika la ndege linalofanya biashara katika eneo la Mombasa, Kisumu na kwingineko linadai gharama kubwa kuliko wengine wote. Kwa mfano, tikiti ya economy leo kutoka Mombasa kuja Nairobi asubuhi iliikuwa shilling elfu thelathini. Hiyo ni karibu dola mia tatu ambazo zinaweza kukupeleka kutoka Mombasa hadi London ama Frankfurt kwa ndege zinazotoka nje. Kufungwa huku kwa biashara na kuwapa nafasi Kenya Airways pekee ni ‘monopoly’. Inalemaza uchimi wa Kaunti za pwani. Malindi vile vile ina kiwanja cha ndege ambacho ni cha kiwango cha kimataifa kinacholemaa kwa sababu hiyo. Uwanja wa ndege wa Eldoret kule Uasin-Gishu una ndege nyingi za mizigo. Watu wengi wanapeleka mizigo yao kupitia kule kwa sababu ni rahisi kufanya clearance na kuchukuwa mizigo yao. Hatuoni sababu gani viwanja vya ndege vya kimatiafa vya Moi, Malindi na Kisumu haviwezi kuruhusiwa kupokea ndege za kigeni kulingana na ile tunaita ‘open skies policy’. Hatuwezi kuendelea kama Afrika iwapo tumefunga njia, anga na bandari zetu na hatuwezi kupokea. Mhe. Spika wa Muda, bandari ya Mombasa hupokea maelfu ya meli kila mwaka. Meli hizi zinatoka nchi za kigeni zinaleta mizigo na kubebe mingine kutoka Mombasa. Hatuoni sababu ya Uwanja wa Moi Mombasa kutotumika kwa swala hilo. Pili, Uchumi Samawati ni jambo ambalo halikutajwa katika hotuba ya Rais, lakini ni muhimu sana kufufua uchumi wa Kaunti za pwani. Tunao ufuo wa bahari kutoka Lungalunga ama Vanga kusini mpaka Kiunga kaskazini. Sisi kama wenyeji wa eneo lile hatujaweza kupata faida zake kamilifu. Kwa mfano, uvuvi wetu bado ni ule wa kiasili. Unavua kutumia vidau, mshipi moja ama nyavu ndogo ambao hausaidii kupata samaki wa kutosha kukuwezesha kulisha familia na kuuza ili kupata mapato ya kukusaidia na familia yako. Lazima watu wawekeze katika Uchumi Samawati. Unaweza kutuletea utalii na biashara ya samaki, kawi ya upepo wa bahari na vile vile mafuta na vitu vingine ambavyo vinapatikana katika bahari hii. Katika swala la sheria yani ‘rule of law’, kuna dalili zinazoonyesha kua serikali hii haitaweza kuheshima uhuru wa sheria. Jambo la kwanza ambalo tuemona ni kuwa mahakama imerushiwa vishawishi kadhaa ambavyo vinavyonyesha kwamba serikali hii iko tayari kuhujumu uhuru wa mahakama. Kwa mfano, siku ya pili alipochaguliwa Rais Ruto, tuliona mambo ya kuapishwa harakaharaka kwa majaji sita yalifanywa haraka ambao walikuwa wamezuiliwa siku za awali. Tumeona pia kuna mipango ya kuongeza ruzuku kwa mahakama kwa jumla. Bw. Spika wa Muda, mwisho ni kuwa Rais alipowasili, jambo la kusikitisha ni kuwa Jaji Mkuu na Naibu wake walikuwa wamesimama kwa msitari hapo nje kumpokea Rais. Hili sio jambo la kawaida. Hata wewe nyumbani kwako, huwezi kualika wageni halafu wageni wa kwanza wakishaingia, unawachukua waandamane na wewe mwenyeji kwenda kuwapokea wageni wengine. Mgeni wako ni wako, mpokee wewe binafsi. Ilikuwa makosa Bunge letu kuwasimamisha wakuu wa Taasisi huru katika nchini, kulingana na kanuni za kumpokea Rais. Mwaka uliopita, kulikuwa na mjadala kuhusu watu fulani ambao walikuwa wamechaguliwa katika nyadhifa za uongozi. Wengine wao walikuwa na tashwishi huku wakiwa wameshitakiwa mahakamani kwa ufisadi na jinai. Waliombwa wajiondoe katika nyadhifa zao kwa muda, hadi makosa yao yathibitishwe ama yaondolewe. Mjadala huo umebadilika sasa. Sasa imekuwa ya kwamba, watu wanachaguliwa kuchukua nyadhifa Serikalini ilihali bado wako na kesi mahakamani. Hii sio dalili nzuri. Inamaanisha tumeanza kupuuza polepole Sura ya Sita ya Katiba inayohusu maadili. Hivi vigezo viwili vinaonyesha kwamba haki haitakuwa inatendeka katika nchi yetu. Katika Bunge la Seneti, tumeona Upande wa Wachache umehujumiwa. Maseneta waliochaguliwa kutoka sehemu hizo wametekwa. Hii sio dalili nzuri katika maswala ya uhuru wa mahakama, taasisi huru kama vile Bunge na pia tume huru za kutetea haki za binadamu. Jambo la mwiso ambalo ningependa kugusia ni maswala ya mbegu zilizobadiliswa na kuweza kuzaa kwa wingi. Kwa Kiingereza tunaita Genetically Modified Organisms (GMO). Ni hatari kwa nchi yetu kukubali mbegu hizi. Mfano ni hivi majuzi tu ambapo kina dada walianza mtindo wa kudungwa dawa za kuongeza makalio yakuwe makubwa. Hili limeleta hatari kwa wanadada wengi. Juzi katika vyombo vya habari, tumemwona mwana mitindo, Vera Sidika, akizungumzia kuhusu matibabu aliyopitia ili kurekebisha makalio yake. Bw. Spika wa Muda, maswala ya GMO ni kama hivyo. Hatutakuwa na uhakika wa mbegu ambazo sasa tutakuwa tunakula. Hatujui zitaathiri miili yetu kwa njia gani. Tumeshuhudia mkurupuko wa visa vya kansa, maradhi yasiyo na tiba na maradhi mengine ambayo hayaeleweki. Kwa hivyo, hatujafikia kiwango cha kupokea vyakula vya GMO. Hatuna sheria ama kanuni nzuri ambazo zinaweza kudhibiti maswala ya vyakula hivi. Afadhali tubaki na njaa yetu, kuliko kula hivi vyakula vya GMO ambavyo vitatusababishia madhara zaidi. Kwa mfano, mara nyingi hapa Kaunti ya Kitui, watu wamekula mahindi yenye sumu ya ukoga wa mwani au aflatoxin. Ukila sumu aina hiyo, itakudhuru na hata unaweza kufariki. Kwa sasa, hatuna sheria ama kanuni za kudhibiti vyakula hivi. Kwa hivyo, sio salama kwa wananchi wetu kuruhusiwa kula hivyo vyakula. Sisi ni watu wa Upande wa Upinzani na tuko tayari kupambana na maswala ambayo Serikali italeta katika Bunge hili. Ikiwa ni maswala mazuri, tutayaunga mkono lakini ikiwa yataathiri vibaya umma ama wananchi wetu, tuko tayari kuyapinga na kuhakikisha haki imetendeka.